Mamlaka ya Hali ya Hewa kutoa utabiri wa mvua
MAMLAKA ya Hali ya Hewa (TMA) imesema mifumo ya hali ya hewa inaonesha hali si mbaya, na imeahidi kutoa utabiri rasmi siku ya Jumanne.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Dk Agnes Kijazi wakati akifungua mkutano wa wadau kuhusu athari za utabiri wa mvua za masika za msimu wa Machi hadi Mei, mwaka huu kwa sekta mbalimbali.
Alisema wamekuwa wakiangalia mifumo ya hali ya hewa na inaonesha kuwa hali si mbaya na wanatarajia kuzidi kuimarika.
“Hali si mbaya sana, ila utabiri utakuaje ndio tutatangaza siku ya Jumanne. Tumeshatazama, tumeona hali ikoje kesho tutaangalia hadi jumatatu na jumanne ndipo tutatoa hali halisi,” alisema Dk Kijazi.
Amesema maeneo mengi ya nchi yameathiriwa na mabadiliko ya hali ya hewa ambayo yanajidhirisha hasa katika kubadilika kwa mtawanyiko wa mvua, misimu ya mvua kuwa mifupi, kupungua kwa wingi wa mvua, kuongezeka joto pamoja na matukio mengine ya hali ya hewa.
Dk Kijazi amesema, msimu wa mvua za vuli uliopita katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba mwaka jana maeneo mengi ya nchi yalipata mvua za chini ya wastani na hiyo ilisababishwa na kuwepo kwa mifumo ya hali ya hewa iliyokuwepo kwa kipindi hicho iliyosababisha ukanda wa mvua kutoimarika katika maeneo mengi ya nchi.
Amesema taarifa sahihi za hali ya hewa ni muhimu na zinahitajika sana hasa wakati huu ili kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.
“Taarifa hizi zimelenga kuwawezesha wadau katika sekta zenu kupanga vyema shughuli zenu za muda mfupi, wa kati na muda mrefu. Wakulima na wafugaji kuweza kupanga kwa uhakika muda wa kuandaa mashamba pamoja na mambo mengine,” amesema.
Amefafanua kuwa, kumekuwa na ongezeko kubwa la uhitaji wa taarifa mahususi za hali ya hewa na ushauri katika jamii hivyo kuongeza uhitaji wa ushirikiano wa pamoja baina ya sekta ya hali ya hewa na sekta nyingine katika kukidhi mahitaji hayo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka hiyo, Dk Burhani Nyenzi amesema mamlaka hiyo inazidi kujikita katika kuhakikisha inatoa taarifa zitakazowezesha wananchi kutumia taarifa hizo.
No comments