Watano mbaroni kwa mauaji ya watu watatu
POLISI mkoani Rukwa inawashikilia watu watano wakituhumiwa kuwaua kikatili watu watatu wa familia moja ambao ni wakazi wa kijiji cha Mfinga kilichopo katika Bonde la Ziwa Rukwa wilayani Sumbawanga kwa kwa kucharangwa na mapanga na mashoka kwa kile kilichoelezwa kuwa ni imani za kishirikina.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, George Kyando, aliwataja marehemu hao kuwa ni Joachim Kayanda (60), mkewe Evelina Mwanakatwe (47) na mtoto wao wa kiume aitwaye Emanuel Kayanda (27) .
Kwa mujibu wa Kamanda Kyando, watuhumiwa hao ambao hakuwa tayari kutaja majina yao kwa hofu ya kuvuruga upelelezi wa kipolisi unaoendelea, wanaendelea kuhojiwa na polisi ambapo watafikishwa mahakamani baada ya upelelezi wa awali wa shauri lao kukamilika .
Alisema mauaji hayo yalitokea Februari 22, mwaka huu usiku wa manane katika kijiji cha Mfinga kilichopo katika Tarafa ya Mtowisa iliyopo katika Bonde la Ziwa Rukwa wilayani Sumbawanga.
Akisimulia mkasa huo, Kamanda Kyando alisema kuwa usiku huo wa tukio watu wasiofahamika wakiwa na silaha za jadi yakiwemo mapanga, mashoka na marungu walifunga mlango wa nyumba walimolala wanafamilia hao na kuwaua kikatili kwa kuwakata kata kwa mapanga na mashoka.
Alidai kuwa watu hao walifanikiwa kutoroka katoka eneo hilo la tukio muda mfupi baada ya kutenda unyama huo.
“Chanzo cha mauaji hayo ni imani za kishirikina kwani familia hiyo ilikuwa inatuhumiwa kuwa ni washirikina,” alisisitiza.
No comments