Biashara ya bodaboda yapigwa marufuku zanzibar
VIJANA wanaofanya biashara ya kusafirsha abiria kwa kutumia usafiri wa Pikipiki wameiomba serikali ya Zanzibar kubadilisha sheria ili usafiri huo uwe halali kibiashara kama ilivyo kwa vyombo vyingine vya moto.
Wakizungumza na Nipashe kwa nyakati tofauti vijana hao walisema hivi sasa wamekuwa wakifukuzwa na kutoruhusiwa kufanya biashara hiyo ambayo inawasaidia kujiajiri.
Walisema wameamua kujiajiri katika biashara hiyo kutokana na ukosefu wa ajira, lakini pia baada ya kuona kuwepo kwa usumbufu wa usafiri kwa maeneo mbalimbali ya Zanzibar.
Waliongeza kuwa baada ya kuona wananchi wanapata usumbufu mkubwa katika suala la usafiri waliamua kuanzisha biashara hiyo ambayo imekuwa ikiwasaidia kujikomboa kiuchumi na kuondokana na umaskini.
Kombo Yussuf, ni miongoni mwa vijana waliojiajiri katika kusafirisha abiria kwa kutumia Pikipiki aliomba Serikali kubadilisha sheria ili usafiri huo uruhusiwa kisheria Zanzibar kama ilivyo kwa Tanzania bara.
“Hakuna lisilowezekana kama sheria hivi sasa hairuhusu inatakiwa ibadilishwe ili usafiri huo uruhusiwe maana utapunguza tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana”alisema Kombo.
Ofisa Mipango wa Idara ya Usafiri na Leseni Zanzibar, Haji Ali Zuberi alisema kwa mujibu wa sheria ya Zanzibar biashara ya usafiri wa Pikipiki hauruhusiwi na atakayaegundulika kufanya biashara hiyo atachukuliwa hatua za kisheria.
“Sheria namba saba ya mwaka 2003 imeainisha usafiri wa barabarani unaoruhusiwa kihalali na usafirishaji wa abiria kwa kutumia Pikipiki ni marufuku,”alisisitiza.
Alisema idara hiyo inakusudia kufanya operesheni maalum ya kuwasaka wanaofanya biashara ya kusafirisha abiria kwa kutumia Pikipiki na atakayebainika atafunguliwa mashtaka.
Alisema usafiri huo unaweza kusababisha madhara mbalimbali ikiwemo ajali na vifo pamoja na ujambazi kama ilivyo kwa Tanzania bara.
Aliwataka vijana waliojiajiri katika biashara hiyo kuacha mara moja na kutafuta ajira zingine ambazo zinakubaliwa kisheria ili kuepukana na athari mbalimbali ambazo zinaweza kutokea.
No comments