Urusi na China zatumia kura turufu kuisaidia Syria

Urusi na China zimetumia kura turufu kuzuia jaribio la Umoja wa Mataifa la kutaka kuiwekea vikwazo serikali ya Syria.

Marekani, Uingereza na nchi nyengine katika Baraza la Usalama, zilitaka kuiadhibu Damascus kwa tuhuma za kutumia silaha za sumu katika maeneo ya waasi.

Ni mara ya saba sasa Urusi inatumia kura yake ya VETO kuikinga serikali ya Rais Assad na tuhuma za kimataifa.

Katika hotuba yake iliyojawa hisia kabla ya kura, balozi wa Uingereza katika Umoja wa Mataifa, Matthew Rycroft, alisimulia kifo cha mwathirika mmoja ambae alipelekwa katika hospitali baada ya shambulio la gesi yenye sumu.

Hata hivyo, kwa upande wake, balozi wa China katika Umoja wa Mataifa, Liu Jieyi, ameliambia Baraza la Usalama kwamba bado hakuna vilelezo kwamba serikali ya Syria imetumia silaha za kemikali.

Naye Rais Vladmir Putin amesema vikwazo vitazuia jitihada za mazungumzo ya amani yanayoendelea Geneva baina ya serikali na wapinzani wake.

Marekani imesema Urusi na China zimekataa kuwajibisha vikosi ambavyo viliangusha gesi za sumu na kusababisha vifo vya wanaume, wanawake na watoto.

No comments

Content by MwasebaINFO.All RIghts Reserved. Powered by Blogger.