HEKARI 1500 ZA RC MAKONDA ZAZUILIWA



WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, amemtikisa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwa kuzuia ekari 1,500 za ardhi alizopewa na Kampuni ya Azimio Housing Estate (Ahel) na kusema kuwa ni mali ya Serikali.

Uamuzi huo wa Serikali umekuja siku chache baada ya Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Mohamed Iqbal kutangaza kumpa Makonda ekari hizo zilizoko katika eneo la Kisarawe II, Wilaya ya Kigamboni ili kuendeleza viwanda vidogo vidogo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Lukuvi alisema Makonda alidanganywa kwa sababu wananchi walishashinda kesi mahakamani ambayo ilifunguliwa na Iqbal.

“Eneo lile ni la Serikali si la yule mtu aliyejitangaza anampa Makonda na kwa sababu amemdanganya na mimi ndiye msimamizi wa ardhi, nitamsaidia Makonda kuchukua hatua ili watu wasijipendekeze kusafisha maovu yao kwa kutumia migongo ya viongozi.

“Hadi siku ile (Jumanne iliyopita) alipokuwa anajipendekeza kwa Makonda, ardhi ile haikuwa yake, wananchi walishashinda mahakamani kwa sababu hakuwa na vielelezo.

 “Ukimdanganya Mkuu wa Mkoa umeidanganya Serikali, Makonda hakuomba ile ardhi ila yeye (Iqbal) ndiye alikwenda kumgawia na amemgawia akijua kwamba alishashindwa,” alisema Lukuvi.

Alisema tayari Serikali imeanza kuwashughulikia wananchi ili wapate haki yao na eneo la viwanda libaki na kwamba wazo la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ndiyo wazo lao.

Lukuvi alisema eneo hilo litabaki kuwa la viwanda baada ya kuondoa matumizi mengine ya wananchi na kwamba eneo jingine litakuwa la dampo.

JINSI ALIVYOPEWA

Februari 21, mwaka huu mfanyabiashara huyo alisema aliamua kutoa eneo hilo kuunga mkono juhudi za Rais Dk. John Magufuli ambazo zinalenga kukuza sekta ya viwanda nchini.

“Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, aliniomba nisaidie katika suala hili la kuendeleza viwanda na mimi nimekubali kutoa ardhi kwa sababu wafanyabiashara ndogo ndogo wanakua na ili waweze kufanikiwa zaidi ni lazima kuweka mazingira mazuri ya kufanyia shughuli zao,” alisema Iqbal.

Kwa upande wake, Makonda alisema eneo hilo litagawanywa kwa wilaya zote za Mkoa wa Dar es Salaam na kwamba wanatarajia ujenzi utaanza Aprili.

“Changia ukijijua mikono yako ni misafi, kwa sababu ukichangia wakati mikono yako ni michafu, hiki si kichaka cha kujificha. Mimi bado nitakushughulikia tu kwa sababu safari yangu ya kwenda mbinguni bado haijakamilika,” alisema Makonda.


No comments

Content by MwasebaINFO.All RIghts Reserved. Powered by Blogger.