Vita dhidi ya madawa ya kulevya Rais Magufuli asema watanzania 1,007 wanaoshikiliwa kwenye magereza mbalimbali duniani serikali haitahusika kuwatetea
Rais Wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk JOHN POMBE MAGUFULI, ameziomba jumuiya za Kimataifa kusaidia katika vita ya dhidi ya dawa za kulevya na kuagiza watanzania 1,007 wanaoshikiliwa kwenye magereza mbalimbali duniani, kuwa serikali haitahusika nao katika kuwatetea.
Rais Magufuli amesema vita dhidi ya dawa za kulevya ni jukumu la Serikali kwa mujibu wa sheria namba tano ya Kupambana na Madawa ya Kulevya ya mwaka 2015, na kuvitaka vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika vita hiyo ili kuokoa vijana ambao wamekuwa waathirika wakubwa wa dawa hizo.
Kauli hizo amezitoa Ikulu jijini Dar es salaam wakati akizungumza na wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama, Baadhi ya Mawaziri wakati wa kuwaapisha mabalozi watatu na Kamishna wa uhamiaji pamoja na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya.
Pia Rais Magufuli ambaye ni Amiri Jeshi mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, amepongeza jitihada zilizoanza nchini za kukabiliana na dawa za Kulevya na kuwataka wananchi kutobeza juhudi zilizoanza kuchukuliwa, huku akitaja vijana wa kitanzania ambao wanashikiliwa magerezani nje ya nchi, miongoni mwake 68 wakiwa wamehukumiwa kunyongwa .
Rais Magufuli amevitaka vyombo vya Usalama na serikali yake kwa ujumla kutomwogopa yeyote katika vita dhidi ya dawa za kulevya.
Rais Magufuli amesema nia ya serikali yake ni kuona hata isiposhinda vita ya dawa za kulevya, taifa lifanikiwe kuipunguza biashara hiyo.
Awali Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la kudhibiti Matumizi ya Dawa za kulevya ambaye Pia ni waziri Mkuu wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania, KASSIM MAJALIWA amepongeza wakuu wa mikoa ya Dar es salaam, Mbeya, kilimanjaro, Shinyanga na Mwanza ambao wameanza mapambano dhidi ya dawa za kulevya, na kuongeza kuwa serikali haitamwacha yeyote atakayejihusisha na Ulimaji, usafirishaji, usambazaji na uuzaji wa dawa za Kulevya nchini.
Katika Hatua nyingine Rais Magufuli amemtaka Kamishna Jenerali wa Uhamiaji kufanya mabadiliko makubwa ndani ya ofisi hiyo hasa kitengo cha fedha, ili kudhibiti mapato ya serikali pamoja na suala la uhamiaji haramu na utoaji wa hati hewa za kusafiria .
Wakizungumza na waandishi wa Habari juu ya Matarajio yao katika nafasi mpya za kazi walizoteuliwa na kuapishwa na Rais, baadhi yao wanaoeleza zaidi.
Katika Hafla ya hiyo, Rais Pia aliwaapisha mabalozi wa Tanzania wanaokwenda kushika wadhifa huo katika nchi ya Ageria ambaye ni OMAR YUSUF MZEE, nchini ubelgiji alieapishwa kushika wadhifa huo ni JOSEPH EDWARD SOKOINE na Grace ARON ameapishwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini UGANDA.
No comments