Jaji Chande Apewa Kazi Umoja wa Mataifa UN


Jaji Mkuu mstaafu Othman Chande ameteuliwa kuongoza jopo la wataalamu watakaochunguza mazingira yaliyosababisha ajali ya ndege iliyomuua aliyekuwa katibu mkuu wa umoja huo, Dag Hammarskjold.

Uteuzi huo wa jaji mkuu mstaafu umefanywa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres.

Hammarskjold alipoteza maisha katika ajali ya ndege iliyotokea Zambia mwaka 1961 wakati akitokea Congo ambayo ndiyo kwanza ilikuwa imepata uhuru.

Hammarskjold alikuwa nchini humo kwa ajili ya ujumbe wa amani.

Naibu msemaji wa UN, Farhan Haq amesema Chande ataongoza jopo hilo ambalo litakuwa na kazi kupitia taarifa zilizoandaliwa na wachunguzi waliopewa jukumu na katibu mkuu mstaafu, Ban Ki-moon.

Uchunguzi huo unafuatia azimio la Umoja wa Mataifa lililopitishwa na Baraza Kuu ambalo lilipendekezwa kufanyika uchunguzi wa kina kubaini mazingira ya ajali hiyo.

Awali, kulikuwa na ripoti kuwa Uingereza na Marekani zilikuwa zimegoma kutoa baadhi ya taarifa muhimu kuhusu tukio hilo, huku Afrika Kusini ikilalamikiwa kwa kushindwa kutoa majibu kwa baadhi ya hoja.

Ripoti iliyotolewa na wataalamu huru waliochunguza ajali hiyo inaeleza kuwa Hammarskjold aliuawa baada ya kunusurika kwenye ajali hiyo. Kumekuwa na taarifa kuwa ndege hiyo ilishambuliwa.

Jopo hilo linaloongozwa na Chande linatarajia  kuanza kazi mara moja na kwamba litakuwa na jukumu la kupitia nyaraka zote, ikiwamo ripoti ya kurasa 99 iliyoandaliwa na wataalamu wa awali waliochunguza mazingira ya ajali hiyo.

No comments

Content by MwasebaINFO.All RIghts Reserved. Powered by Blogger.