Cameroon Yatawazwa Mabingwa wa Afcon 2017






Timu ya Taifa ya Soka ya Cameroon imetawazwa kuwa mabingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) mwaka 2017 baada ya kuilaza timu ya Taifa ya Misri kwa mabao 2-1, yaliyofungwa na Nicolas N'Koulou na Vincent Aboubakar.

Cameroon imepata ubingwa huo katika fainali za mashindano hayo yaliyofanyika nchini Gabon, ukiwa ni ubingwa kwa mara ya tano na ni mara ya kwanza tangu mwaka 2002.

Katika mtanange huo uliovuta hisia za mashabiki na wapenzi wengi wa soka, Misri ndiyo ilianza kutikisa nyavu za Cameroon baada ya Mohamed Elneny kufunga goli kwa shuti kali katika dakika ya 21.

Hata hivyo, katika dakika ya 58, N'Koulou aliamsha matumaini ya Cameroon kutwaa ubingwa huo, baada ya kuisawazishia timu yake kwa kichwa, kabla ya Aboubakar kuihakikishia ubingwa kwa kupachika wavuni bao la pili katika dakika ya 88 na hivyo kuzamisha kabisa jahazi la Misri.

Ubingwa wa mwaka huu kwa Cameroon unaandika rekodi mpya na ya kwanza baada ya timu hizo kukutana katika hatua ya fainali mwaka 1986 na 2008, ambazo zote Misri iliibuka mbabe.

No comments

Content by MwasebaINFO.All RIghts Reserved. Powered by Blogger.