Baadhi ya wanafunzi wabainika kufaulu na kujiunga kidato cha kwanza wakiwa hawajui kusoma na kuandika wilayani Longido

Serikali wilayani Longido imeiagiza idara ya elimu wilayani humo kuandaa mtihani wa kuwapima wanafunzi wote waliofaulu mtihani wa darasa la saba na kujiunga na  kidato cha kwanza  baada ya  kubaini  uwepo wa wanafunzi walioingia sekondari wakiwa hawajui kusoma na kuandika.

Agizo hilo linatolewa na mkuu wa wilaya hiyo Daniel Chongolo katika kata ya Ketumbeine yalipofanyika maadhimisho ya siku ya taaluma kiwilaya ambapo anaeleza kuwa hali hiyo inazidi kudidimiza elimu katika maeneo hayo ambayo mengi ni ya pembezoni.

Kwa upande wao wazazi wakatupia lawama baadhi ya walimu ambao wamekua na utaratibu wa kuwavusha wanafunzi madarasa bila kukidhi vigezo malalamiko ambayo  afisa   wa elimu ya msingi Natalia Laiser anasema yameshaanza kufanyiwa kazi kwa kutenga madarasa maalum  kwa watoto wenye uelewa wa taratibu.

Jumaa Mhina ndiye mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo ya Longido anasema kwa sasa wameanza kutoa motisha kwa walimu wa shule za pembezoni zinazofanya vizuri na wanaendelea kushirikiana na wadau katika kuhakikisha upatikanaji wa  chakula ili kupunguza utoro.

No comments

Content by MwasebaINFO.All RIghts Reserved. Powered by Blogger.