Wezi waiba laptop ya skrini tatu Las Vegas Marekani

Wezi waiba laptop ya skrini tatu Las Vegas Marekani


 Razer walidai laptop hiyo ya skrini tatu waliyoipatia jina Project Valerie ni ya kwanza ya aina yake duniani

Kampuni ya Razer imetangaza kwamba mbili kati kompyuta mpakato maarufu kama laptop ambazo zina skrini tatu badala ya moja ambazo zilikuwa zimeundwa na kampuni hiyo zimeibiwa.

Laptop hizo za maonesho, ambazo sana zinawalenga watu wanaopenda michezo ya kompyuta, ziliibiwa wakati wa maonesho ya teknolojia ya CES yaliyokuwa yakifanyika mjini Las Vegas, Marekani.

Kompyuta hizo zilionyeshwa hadharani kwa umma mara ya kwanza wakati wa maonesho hayo.

Kampuni ya Razer inasema ilikuwa imebeba kompyuta tatu za aina hiyo lakini waligundua Jumapili kwamba laptop mbili kati ya hizo zilikuwa zimetoweka kutoka kwenye kibanda cha kampuni hiyo siku ya Jumapili.

Skrini zote tatu za laptop hiyo, ambayo imetajwa kuwa ya kwanza ya aina yake duniani, ni za kiwango cha kuonyesha pikzeli 4,000 (4k) na ni za ukubwa wa inchi 17 (43cm).

Skrini mbili huchomoza kila upande kutoka kwa skrini kubwa ya kati, moja kwa moja.

Afisa mkuu mtendaji wa kampuni hiyo Min-Liang Tan amesema kisa hicho kinachukuliwa "kwa uzito sana".

Msemaji wa Razer amesema kampuni hiyo imeahidi kutoa $25,000 (£20,600) kwa atakayetoa habari za kusaidia "kutambuliwa, kukamatwa na kuadhibiwa" kwa waliohusika katika uhalifu huo.

"Maafisa wetu walifanya kazi kwa miezi mingi kuunda kompyuta hizi," Bw Tan alisema kupitia ukurasa wake rasmi wa Facebook.

"Huu ni udanganyifu, ni wivi na haujatufurahisha. Yeyote aliyefanya hivi bila shaka ni mtu mjanja sana."

Msemaji wa Chama cha Watumiaji wa Teknolojia, shirika linaoandaa maonesho ya CES, ameambia BBC kwamba ni kweli kisa cha kuibiwa kwa laptop hizo mbili kimeripotiwa

Razer, kampuni ambayo ina makao makuu yake California, ilianzishwa na mjasiriamali kutoka Singapore Min-Liang Tan.

Ni kampuni inayosifika na kuheshimiwa sana katika tasnia ya michezo ya kompyuta.

Mashabiki wa michezo ya kompyuta duniani walikuwa wamefurahia sana habari za kuzinduliwa kwa kompyuta hiyo mpya ya skrini tatu ambayo imepewa jina Project Valerie.

No comments

Content by MwasebaINFO.All RIghts Reserved. Powered by Blogger.