Tucta kutangaza mapendekezo kima cha chini cha mshahara
SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), limeahidi kutangaza kwa serikali mapendekezo yake ya kima cha chini cha mishahara kwa watumishi wa umma na sekta binafsi wakati wowote kuanzia sasa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Rais wa Tucta, Tumaini Nyamghokya, mapendekezo hayo ya kima cha chini na nyongeza ya mishahara yanaendelea kufanyiwa kazi na wataalamu wao.
“Tunataka mapendekezo hayo mapya yamfikie Rais John Magufuli mapema kabla ya maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani, Mei Mosi,” alisema Nyamghokya.
Nyamghokya aliyasema hayo juzi alipokuwa akifungua Mkutano Mkuu wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini wa Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO).
Alisema baada ya mapendekezo hayo kutoka, Tucta itazungumza na kiongozi huyo wa nchi ili kuyatetea kwa kuwa yanalenga kuongeza motisha kwa wafanyakazi nchini.
Alisema kwa jinsi hali ilivyo hivi sasa (hakuitaja hali hiyo) wana matarajio Rais atayachukua mapendekezo yao na kuyafanyia kazi. Pamoja na mapendekezo hayo, kiongozi huyo wa Tucta alisema wafanyakazi wanaelemewa na mzigo mkubwa wa kodi zinazokatwa katika mishahara yao.
“Kodi hizo zimeleta manung’uniko kwa watumishi hasa wenye mishahara ya kima cha kati na cha juu kwa kuwa makato yao ni makubwa,” alisema.
Alisema Tucta inataka Rais awatetee wafanyakazi kama alivyoonesha kuwatetea wafanyabiashara ndogo (machinga) waliotaka kuondolewa na mamlaka katika maeneo yao bila kuoneshwa maeneo mapya ya kwenda. Alisema wafanyakazi wanaunga mkono juhudi mbalimbali zinazofanywa na Rais katika kushughulikia changamoto za nchi.
No comments