RUSHWA YA NGONO BADO NI TISHIO NCHINI
Rushwa ya ngono bado tishio nchini
SUALA la rushwa ya ngono limeendelea kuwa tishio nchini hadi kusababisha wanawake wengi kujiengua katika nafasi zao.
Hayo yamebainishwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan wakati akifungua Mkutano wa Nane wa Chama cha Majaji Wanawake Tanzania (TAWJA), uliofanyika Dar es Salaam jana.
Samia alisema ni jambo la kuvunja moyo, kuona kwamba katika Karne ya 21 suala la rushwa ya ngono, linaendelea na kusababisha wanawake wengi kujiengua katika nafasi zao.
Makamu wa Rais alionya juu ya vitendo hivyo vya rushwa ya ngono, vinavyofanywa na baadhi ya watendaji wenye madaraka na kusema tabia hiyo ni mbaya na lazima ikomeshwe mara moja katika jamii.
“Matumaini, matarajio na ndoto za wanawake, zimekuwa zikikatishwa na watu wachache ambao ni hatarishi, hivyo tunahitaji kufanya kazi kuhakikisha kwamba tunawasaidia kwa hali na mali kwa sababu wahanga hao wanaweza kuwa mama yako, dada, mke na binti yako,’’ alisema Makamu wa Rais.
Alisema kuwa vitendo hivyo vya rushwa ya ngono, huzuia na kukwamisha juhudi za wanawake kufikia huduma za kijamii na za kiserikali ipasavyo, ikiwemo elimu, ajira na haki kwa ajili ya ustawi wa wanawake.
Makamu wa Rais aliwaagiza majaji na mahakimu wanawake kote nchini, kupambana ipasavyo na kukabili vitendo vya unyanyasaji kijinsia na rushwa ya ngono ili kusaidia wanawake kupata haki zao za msingi bila kubaguliwa katika jamii.
Alisisitiza kuwa atahakikisha kwamba wanawake na watoto, wanapatiwa haki zao kwa uhuru bila ya ubaguzi wala vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi yao.
Samia aliongeza kuwa kuondoa vikwazo vya kisheria kuhusu ukatili na unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya wanawake ni miongoni mwa maeneo makubwa sita katika kuondoa pengo kubwa la kiuchumi.
Alifafanua kuwa serikali inahamasisha kushiriki kutekeleza sheria za kimataifa katika kupambana na unyanyasaji wa kijinsia, rushwa ya ngono na umiliki wa mali dhidi ya wanawake. Samia aliwahimiza majaji hao kutoa hukumu kwa wakati katika kesi wanazoendesha ikiwa ni pamoja na kufuata maadili na kanuni zilizowekwa.
Aidha, aliwataka kuhakikisha kwamba wanatoa bure elimu ya haki za binadamu na ujuzi kwa maofisa wa mahakama, watunga sera na waathirika wa ukatili wa kijinsia. Akitoa takwimu za ushiriki wa wanawake katika nafasi mbalimbali, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman alisema asilimia 44 ya majaji waliopo katika mahakama ni wanawake huku Mahakama Kuu pekee ikiwa na asilimia 47.9 ya wanawake.
Alisema Bunge lina asilimia 46.6 ya wanawake wakati katika nchi jirani ikiwemo Kenya, wana idadi ndogo ya majaji wanawake ambayo ni asilimia 3.3. Jaji Othman alisema kuwa wasajili wa mahakama waliopo, asilimia 34 ni wanawake na kwamba nafasi ya uongozi hususan kwa mahakimu wafawidhi wa mahakama za mwanzo na kati, imeongezeka.
‘’ Malengo yetu kama mahakama ni kuongeza idadi ya wanawake katika mahakama zetu zote, kwani ndio mahitaji na matakwa ya sheria. Pia niipongeze TAWJA ambayo imekuwa ikitoa mchango mkubwa katika mahakama kwa kutoa elimu kuhusu masuala ya kisheria kwa maofisa wa mahakama na wengine wenye uhitaji,’’ alisema Jaji Othman.
Aidha, alisema kuwa kuongeza idadi ya mahakama za mwanzo na za kati ni ishara ya kuongeza huduma za kisheria pamoja na utoaji wa elimu, itakayosaidia kuiboresha mahakama pia.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TAWJA, Jaji Imani Aboud alisema kuwa mkutano huo umekuwa ukifanyika kila mwaka na lengo ni kuzungumzia masuala mbalimbali, ikiwemo mafanikio, changamoto na malengo yao ya baadae.
Alisema kuwa miongoni mwa changamoto zinazowakabili ni pamoja na rushwa ya ngono, ambayo licha ya mwanamke kuwa na haki ya kupata kazi, huombwa rushwa hiyo ili kumrahisishia upatikanaji wake.
‘’Tumejipanga kufanya kazi kwa mujibu wa sheria pamoja na kutoa elimu kuhusu sheria zilizopo na kuwasaidia wanawake na jamii kwa ujumla, kazi hii itafanyika kwa kadri serikali ya awamu hii inavyotaka,’’ alisema Jaji Aboud.
No comments