MWANZA: WATANO MBARONI KWA TUHUMA ZA KILIMO CHA BANGI

WATU watano wanashikiliwa na Polisi wilayani Sengerema mkoani Mwanza kwa tuhumza za kujihusisha na kilimo cha bangi.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema jana kuwa watu hao walikamatwa Januari 4 mwaka majira ya saa tatu usiku katika Kijiji cha Nyabutanga Tarafa ya Buchosa wilayani Sengerema.

Alisema watu hao walikamatwa baada ya polisi kupata taarifa kutoka kwa raia wema, ambao walitoa taarifa za watu hao kujihusisha na kilimo cha bangi kijijini hapo.

Polisi kwa kushirikiana na wananchi walipata jumla ya miche ya bangi 17,794 kwenye mashamba yao. Aliwataja waliokamatwa kuwa ni Julius Ndalo(80), George Julius(23), Joseph Julius(28), Mabula Julius (17) naTabu Dawa(34), wote wakazi wa Kijiji cha Nyabutanga.

“Baada ya Polisi kupata taarifa juu ya kilimo hicho cha bangi kutoka kwa raia wema, walikwenda kijijini hapo na kukuta mashamba mawili yenye ukubwa wa ekari tatu yakiwa yamepandwa bangi pamoja na mahindi,” alisema.

Kamnda Msangi alisema polisi waling’oa miche yote usiku siku hiyo. Alisema watuhumiwa wanahojiwa na polisi na uchunguzi utakapokamilika watafikishwa mahakamani.

“Bado tunaendelea na upelelezi wa kuwatafuta watu wengine wanaojihusisha na kilimo cha bangi, natoa wito kwa wakazi wa mkoa huu waache kufanya kazi ambazo sio halali, zinazoenda kinyume cha sheria za nchi,”alisema.

No comments

Content by MwasebaINFO.All RIghts Reserved. Powered by Blogger.