JOTO LAZUA SINTOFAHAMU MOSHI
Moshi.Taarifa za wiki nzima za Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) zilizopo kwenye tovuti yake zinaonyesha kiwango cha joto cha maeneo ya Moshi na Same mkoani Kilimanjaro kinaizidi mikoa iliyoko ukanda wa pwani ukiwamo Dar es Salaam.
Hali hiyo imewafanya wakazi hususan wa mjini Moshi na vitongoji vyake kuwa katika hali ya sintofahamu kutokana na ongezeko hilo la joto na la vumbi jingi.
Viwango vya juu vya joto kwa mikoa iliyopo pwani ya Bahari ya Hindi kwa jana na juzi ni Dar es Salaam (34), Tanga (34), Pwani (34), Mtwara (31), Kusini Pemba (31) na Kaskazini Unguja (34).
Mchungaji wa Usharika wa Karanga wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Fred Njama alisema ongezeko la joto limechangiwa na uharibifu wa mazingira unaofanywa na wananchi kwenye maeneo ya vyanzo vya maji na misitu.
Taarifa za TMA ambazo hutangazwa na vituo mbalimbali vya televisheni, zinaonyesha kiwango cha juu ni nyuzi joto 35 katika mji wa Moshi uliopo kilomita zisizozidi 30 kutoka Mlima Kilimanjaro.
Mtaalamu wa mabadiliko ya tabianchi, Profesa William Makundi alisema tatizo kubwa zaidi ni hewa ya ukaa inayoharibu tabaka la ozoni na tani bilioni 50 za hewa hiyo huzalishwa kila mwaka duniani.
No comments