Farid Mussa aanza kazi Hispania
HATIMAYE winga wa kimataifa wa Tanzania, Farid Mussa amepewa leseni ya kucheza soka nchini Hispania na Shirikisho la Soka la nchini humo (RFEF).
baada ya kutolewa kwa leseni hiyo, winga huyo wa Azam anayecheza kwa mkopo kwenye klabu ya Deportivo Tenerife ameanza kazi rasmi ya kuitumikia timu yake hiyo.
Akizungumza na Nipashe jana kwa simu kutoka Tenerife, Farid alisema kwamba amepangiwa kuanza kuchezea kikosi cha U23 ili kupata uzoefu kabla ya kupandishwa kikosi cha kwanza kinachocheza Ligi Daraja la Kwanza nchini humo, maarufu kama Segunda.
“Nimepatiwa leseni na nimepelekwa Tenerife B ili nikapate uzoefu kwanza na Jumamosi (leo) natarajia kucheza mechi yangu ya kwanza dhidi ya timu inaitwa Vera,”alisema Farid.
Farid amejiunga na klabu hiyo ya mji wa Santa Cruz de Tenerife, kwa mkopo wa muda mrefu tangu Desemba mwaka jana.
Azam imemtoa kwa mkopo Farid kwa makubaliano maalum baada ya winga huyo kufuzu majaribio katika klabu hiyo Aprili mwaka jana alipokwenda na Mkurugenzi wa klabu yake, Yussuf Bakhresa.
No comments