Afa baharini akivua pweza

WAKAZI wawili wa mkoani Tanga wamekufa maji akiwemo mvuvi Mbayai Hassan (20) mkazi wa Tongoni ambaye alikosa pumzi wakati akivua samaki aina ya pweza.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba amebainisha hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana.

Alisema wakazi hao walikufa maji kwa nyakati na katika maeneo tofauti mkoani Tanga.

“Hassan, ambaye alikuwa akijishughulisha na uvuvi wa pweza katika Bahari ya Hindi ni mkazi wa kata ya Tongoni, Tanga na alikutwa na tukio hilo lililosababisha kifo chake jana,” alisema.

“Kwa mujibu wa mashuhuda walisema alikufa baada ya kuzama ndani ya jabali la miamba ya bahari ili kusaka samaki huyo lakini wakati akiendelea na harakati hizo ndipo alikosa pumzi na kupoteza uhai papo hapo,” alisema.

Katika tukio jingine, lililohusisha mtoto aitwae Bakari Meja (15), Kamanda alisema lilitokea wilayani Kilindi, Januari 20 mwaka huu wakati alipokuwa akiogelea baada ya muda wa masomo.

“Meja alikuwa ni mwanafunzi wa darasa la nne katika shule ya msingi Lomwe iliyopo wilayani Kilindi wakati akiogelea katika lambo la kunywesha mifugo ndipo maji yalimzidi nguvu na kufa”.

Aidha, alisema uchunguzi wa polisi kuhusu matukio hayo umekamilika na tayari miili ya marehemu hao imekabidhiwa kwa ndugu zao kwa ajili ya maziko.

No comments

Content by MwasebaINFO.All RIghts Reserved. Powered by Blogger.