HAKI ZA MWANAMKE KATIKA NDOA KWA MUJIBU WA SHERIA YA NDOA YA JAMUHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
SHERIA YA NDOA NA TALAKA
7.0 HAKI ZA MWANAMKE KATIKA NDOA
7.1 Usawa
Sheria ya ndoa katika kifungu cha 56 inatamka bayana kwamba mwanamke aliyeolewa ana haki sawa katika kupata, kumiliki na kutumia mali yake kama ilivyo kwa mwanaume. Kwa ndoa za wake wengi, wanawake katika ndoa hizo wana haki sawa. Pia kifung cha 66 kinakataza mwanandoa yeyote kumpiga mwenziwe kwa sababu yoyote ile.
7.2 Matunzo
Kifungu cha 63 kinatamka kwamba mume ana wajibu wa kumtunza mkewe kwa kumpa mahitaji yote muhimu katika maisha kama mavazi, chakula na malazi kulingana na uwezo wake. Mke pia atakuwa na wajibu huo ikiwa tu mume kwa sababu ya ugonjwa hawezi tena kufanya kazi yoyote. Na kama mume hatekelezi wajibu huo kwa makusudi mahakama chini ya kifungu cha 115 yaweza kumwamuru kutekeleza wajibu huo.
7.3 Kumiliki Mali
Mke ana haki ya kumiliki mali aliyoipata kabla ya ndoa. Ndoa haiwezi kuwa kigezo cha lazima cha kubadilisha umiliki wa mali ya mwanandoa isipokuwa tu kama wenyewe wamekubaliana hivyo na pia haimzuii mwanandoa kujipatia na kumiliki mali yake binafsi akiwa katika ndoa. Kifungu cha 58 kinaeleza haki hiyo.
7.4 Kuishi katika nyumba ya ndoa
Mke ana haki ya kuishi katika nyumba ya ndoa. Kifungu cha 59 kinaeleza kwamba nyumba ya ndoa ni ile ambayo wanandoa wanaishi. Hii inaweza kuwa nyumba waliyojenga au ya kupanga. Na kama nyumba ya ndoa ni ya kujengwa na wanandoa wenyewe, basi hakuna mwenye mamlaka ya kuiuza, kuipangisha au kuiweka rehani bila idhini ya mwanandoa mwenzake.
7.5 Kukopa
Mke ana haki ya kukopa kwa jina la mume wake au kuuza vitu vya mume kwa lengo la kujipatia
mahitaji ya lazima ya familia.
7.6 Uhuru wa kuishi popote
Endapo mume atafariki kifungu cha 68 kinampa mjane haki ya kuamua akaishi wapi na asiolewe au aolewe na mtu ampendaye bila kuingiliwa na mtu au kufungwa na mila yoyote.
7.7 Kupata haki ya jasho lake
Mke ana haki ya kupata haki ya jasho lake alilochangia kwenye mali iliyopatikana wakati wa ndoa iwapo ndoa itavunjika kama inavyoelezwa katika kifungu cha 114.
Happy International Women's Day
No comments