Serikali yaeleza kwa nini wizara zinatumia majengo ya UDOM

Serikali imesema uamuzi kuyatumia majengo ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kama ofisi za baadhi ya wizara zake hautaathiri shughuli za kitaaluma katika taasisi hiyo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama amesema chuo hicho kina majengo mengi ya ziada ambayo kwa sasa hayatumiki.

Waziri Mhagama ametoa ufafanuzi huo, bungeni mjini Dodoma mapema leo, baada ya Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Suzan Lyimo kuhoji sababu za Serikali kuhamishia ofisi zake na makazi katika baadhi ya majengo ya UDOM.

Katika swali hilo la nyongeza, Lyimo alitaka kujua ikiwa Serikali imekurupuka katika uamuzi wake wa kuhamishia ofisi zake katika mji huo uliopo katikati ya nchi ama la.

Waziri Mhagama ametaka wizara nyingine kufanya uamuzi wa kuhamia Dodoma na kutumia majengo ya UDOM kwani serikali ilijenga majengo mengi ambayo hayatumiki kwa sasa.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Angellah Kairuki alihamia mjini Dodoma, ikiwa ni utekelezaji wa tamko la Rais John Magufuli la kuhamishia shughuli za serikali makao makuu ya nchi.

No comments

Content by MwasebaINFO.All RIghts Reserved. Powered by Blogger.