Serikali Yaeleza Hatua Iliyofikiwa Kuhusiana na Walimu Waliompiga Mwanafunzi Mbeya


Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni ametolea ufafanuzi kuhusu hatua inayochukuliwa na vyombo vya dola dhidi ya watu wanaohusika na vitendo vya unyanyasaji vikiwemo kupiga watu.

Naibu waziri huyo ametoa ufafanuzi huo Jumatano hii mjini Dodoma kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani, wakati alipokuwa akijibu swali la mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi.

Mbilinyi aliuliza, “Kumekuwa na tabia za watu kupiga watu wengine, vipigo ambavyo vinafikia kiasi cha utesaji matukio kama yaliyotokea Mbeya Day sekondari kwa mwalimu kumshambulia mwanafunzi lakini na lile la mtu kumtoa macho mwingine tukio lililotokea kule Buguruni, Je, Serikali inachukua hatua gani kwa watu wanaowapiga wenzao bila sababu?”

Mheshimiwa Masauni alijibu, “Ni kweli hivi karibuni kumekuwa na vitendo vya kusikitisha katika nchi yetu na kwa jamii ambavyo ni kinyume na sheria na havikubaliki. Aidha serikali haikubaliani na vitendo vya namna hiyo vinavyofanywa na watu, mtu au kikundi kwani vitendo hivyo ni kinyume na sheria na utaratibu mzima wa haki za binadamu. Serikali kupitia jeshi la polisi imekuwa ikichukua hatua mbalimbali ili kuzuia na kulinda raia na mali zao, aidha serikali kupitia jeshi la polisi tumepokea taarifa za matukio mbalimbali na kuyafanyia uchunguzi wa kina yanapobainika upo ushahidi wa kutosha mtuhumiwa huchukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.”

Aliendelea, “Nichukue fursa hii kuwaasa wale wote wanaokiuka taratibu, kanuni na sheria za nchi waache tabia hiyo mara moja wizara yangu haitakuwa na suluhu kwa mtu yeyote atakayetenda uhalifu huo.”

Ameongeza “Kuhusiana na suala la walimu ambao wamewanyanyasa wanafunzi kwenye shule ya Mbeya day, suala hili ni suala mtambuka kwahiyo ni hatua mbalimbali zinachukuliwa na mamlaka husika kwa upande wa jeshi la polisi kwa kushirikiana na mkurugenzi wa mashtaka ni kwamba kuna hatua zinaendelea kuchukuliwa na pale ambapo uchunguzi utakamilika watafikishwa katika vyombo vya sheria.”

No comments

Content by MwasebaINFO.All RIghts Reserved. Powered by Blogger.