MKE NA MUME JELA MIAKA 55
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewahukumu kwenda jela miaka 55 mume na mkewe, baada ya kupatikana na hatia ya kuratibu na kuuza nyara za serikali, yakiwamo meno na mifupa ya tembo kilo 450.6 yenye thamani ya Sh. bilioni 2.2.
Washtakiwa hao Peter Kabi (45) na mkewe, Leonidia Kabi (46), walikutwa na nyara hizo sawa na tembo 93 waliouawa, wakiwa wamezihifadhi kwenye jeneza na kufunikwa na bendera ya taifa.
Mahakama hiyo chini ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, pia iliamuru nyara walizokutwa nazo washtakiwa zitaifishwe na serikali.
Hakimu Shaidi alisema ushahidi wa mtaalamu wa wanyamapori, Emmanuel Lyimo, ulibainisha kuwa miongoni mwa hasara zinazotokana na kuuawa tembo ni uchumi kushuka.
“Washtakiwa wamekutwa na nyara hizo ambazo ni sawa na tembo 93 waliouawa ... kwa maana hiyo itachukua muda mrefu tembo 93 kuzaliwa,” alisema Hakimu Shaidi na kuongeza:
“Ninyi washtakiwa mmeamua kula matunda ya taifa hili kinyume cha utaratibu ... siyo sahihi mjinufaishe mke na mume, mnastahili kutumikia kifungo cha miaka 15 (kwa) kosa la kwanza, miaka 20 kosa la pili na 20 mingine kwa kosa la tatu na adhabu yote itakwenda sambamba.”
Akizungumzia ombi la Jamhuri kuhusu kutaifishwa nyumba iliyokuwa imehifadhi nyara hizo, Hakimu alisema upande wa Jamhuri uwasilishe maombi yenye vielelezo vya kuthibitisha umiliki halali wa washtakiwa ili mahakama yake itoe uamuzi.
Kabla ya hukumu hiyo, upande wa Jamhuri ukiongozwa na Mawakili wa Serikali, Paulo Kadushi na Elias Athanas uliomba mahakama ijielekeze katika kifungu cha 111 cha Sheria za Wanyamapori kinachotoa masharti ya lazima.
Kadushi alidai kifungu hicho kinaeleza kwamba mtuhumiwa akikutwa na hatia nyara na kitu chochote kilichotumika kuhusiana na nyara hizo, vyote vinataifishwa.
“Mheshimiwa, naiomba mahakama yako ijielekeze kwenye kifungu hicho kwa kutaifisha meno na mifupa ya tembo waliyokutwa nayo washtakiwa na nyumba iliyokuwa imehifadhi nyara hizo kwa kuwa inamilikiwa na washtakiwa wote wawili,” alidai Kadushi.
Upande wa utetezi ulipopewa nafasi ya kuomba kupunguziwa adhabu, ulidai kuwa washtakiwa ni mke na mume ambao wana watoto wawili, wazazi na ndugu wanaowategemea, hivyo uliomba mahakama kuwapunguzia adhabu na kutoitaifisha nyumba wanayoimiliki.
Hakimu alisema kwa kuwa washtakiwa walijipendelea kula keki ya taifa kinyume cha taratibu, watakwenda jela kutumikia kifungo hicho na haki ya rufani kwa upande ambao haujaridhika iko wazi.
AIBU KUBWA
Baada ya kutolewa hukumu hiyo, Mkurugenzi wa Wanyamapori, Alexandra Sogorwa, aliwaambia waandishi wa habari katika viunga vya mahakama hiyo kuwa ni aibu kubwa Tanzania kutoka kuwa na tembo zaidi ya 100,000 miaka 10 iliyopita hadi kufikia 50,000.
“Tusaidiane kupambana kutokomeza ujangili dhidi ya wanyama wetu, wakiwamo tembo," alisema kwa sababu "hali ni mbaya na ni aibu kubwa Mtanzania kuanza kupanda ndege kwenda kuangalia tembo nchini Marekani.”
“Rais ametupa majukumu kupambana na ujangili kiasi kwamba jangili akimuona tembo akimbie ... mahakama imetoa haki kwa pande zote mbili katika kesi hii.”
Naye Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Biswalo Mganga aliyekuwa katika mkutano huo na waandishi wa habari alisema:
"Familia moja inahujumu uchumi wa taifa, wamekutwa na nyara za Sh. bilioni 2.2, kwa kweli hii haiwezi kuvumilika, tusaidiane kutokomeza wahujumu uchumi.
“Washtakiwa walitumia mbinu ya kuweka meno ya tembo kwenye jeneza na kufunika na bendera ya taifa letu wakijifanya wanasafirisha maiti ya askari polisi, kwa kweli hii ni hatari.
"Tusaidiane wanahabari muwaeleze wananchi hasara tunayopata ni yetu sote.”
Biswalo alisema familia moja imeangamiza tembo 93 na kwamba huo ni uhujumu wa hali ya juu.
Katika kesi ya msingi, washtakiwa walidaiwa kuwa Oktoba 27, 2012 katika sehemu tofauti kati ya Dar es Salaam na Iringa, waliratibu kufanyika kwa makosa ya kukusanya na kuuza nyara hizo.
Katika shtaka la pili, ilidaiwa kuwa siku ya tukio la kwanza, eneo la Kimara Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, walikutwa na meno 210 yenye uzito wa kilo 450.6 yakiwa na thamani ya Sh. bilioni 2.1 sawa na tembo 91.
Katika shtaka la tatu, ilidaiwa kuwa siku ya tukio la kwanza, walikutwa na mifupa mitano ya tembo ikiwa na thamani ya Sh. milioni 47.4 sawa na tembo wawili.
No comments