Majaliwa ataka jamii yenye maadili

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema ili kuwa na taifa lenye ustawi, jamii haina budi kuwekeza kwenye makuzi mema ili kuepuka kuwa na taifa la vijana wasio na maadili.

Aidha, amesema serikali inapopambana na uuzaji na utumiaji wa dawa za kulevya, matumizi holela ya pombe za viroba, mimba za utotoni na mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi ili kuboresha huduma za jamii, lengo lake ni kujenga kesho iliyo bora kwa vijana.

Waziri Mkuu aliyasema hayo juzi usiku katika hafla ya chakula cha hisani kwa ajili ya kuchangia maadhimisho ya siku ya Skauti Afrika na miaka 100 ya Uskauti Tanzania, iliyoandaliwa na Chama cha Skauti Tanzania.

Alisema nusu ya Watanzania ni vijana, hivyo ni muhimu kuweka mazingira mazuri kwa ajili yao. Chama cha Skauti kama moja ya taasisi kongwe nchini ni wadau muhimu katika malezi ya vijana.

"Tunaposhuhudia makundi kama Panya Road, ongezeko la vijana wenye uraibu wa dawa za kulevya na ongezeko la mimba za utotoni, sanjari na kuhoji nafasi ya wazazi kwenye malezi ya watoto wetu, tunadhani ni wakati mwafaka pia kwa Chama cha Skauti nacho kujitathmini endapo bado kina ushawishi kama ilivyokuwa miaka ya nyuma na endapo kuna jambo linaweza kufanyika ili kurekebisha hali hiyo," amesema Waziri Mkuu Majaliwa.

Alisema serikali inaendelea kufanya uwekezaji mkubwa kwa ajili ya kuhakikisha kila mtoto mwenye uwezo wa kwenda shule anafanya hivyo, bila kikwazo.

Alifafanua kuwa serikali imekuwa ikitoa Sh bilioni 18.7 kila mwezi ambazo zimesaidia kuondoa ada na michango yote kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne.

Pia alishauri kamati inayoandaa shughulli hizo kubuni njia mbalimbali za kupata michango kama kuwa na mechi za soka, mabonanza ya muziki, bahati nasibu na kampeni za uchangiaji kupitia makampuni ya simu za mkononi.

Aidha, alishauri kamati hiyo kuona uwezekano wa kuunganisha matukio ya maadhimisho ya Miaka 100 ya Skauti Tanzania na Siku ya Skauti Afrika kuyafanya kwa pamoja na kwa bajeti ndogo, ili fedha zitakazookolewa zitumike katika shughuli mbalimbali za kuhamasisha uskauti nchini.

Awali, Rais wa Chama cha Skauti nchini na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako alisema, chama hicho kimekuwa msaada mkubwa katika kuwajenga vijana katika mazingira bora. Alisema lengo la maadhimisho hayo ni kuwahamasisha vijana kuwa raia bora wenye kuwajibika ipasavyo.

Alisema maadhimisho hayo yanahitaji Sh milioni 600 ili yaweze kukamilika, kwani yatashirikisha na nchi nyingine mbalimbali za Afrika na nje ya Afrika.

Katika chakula hicho cha hisani, fedha zilizopatikana kwa ahadi na taslimu ni Sh milioni 265.1, hivyo wananchi kuombwa kuendelea kuwasilisha michango yao kwa ajili ya maadhimisho hayo.

No comments

Content by MwasebaINFO.All RIghts Reserved. Powered by Blogger.