Kampuni ya Mo Dewji, Lamada Hotel ni mdaiwa sugu wa kodi, Wapewa notisi ya siku 14.
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeanza oparesheni maalumu ya kukusanya Kodi ya Pango la Ardhi kutoka kwa wadaiwa sugu wa Makampuni, mashirika ya kiserikali na watu binafsi kwa kuwafuata katika maeneo yao.
Katika hatua ya kwanza Wizara kwa kushirikiana na Manispaa za mkoa wa Dar es salaam imetoa notisi kwa wadaiwa sugu wa kodi ya pango la Ardhi wakiwemo Mohammed Enterprises anaedaiwa Shilingi milioni 73, Lamada Hotel anaedaiwa Shilingi milioni 54, Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA) anaedaiwa Shilingi milioni 144 na Tanganyika Motors anaedaiwa Shilingi milioni 22.
Makampuni hayo yamepewa notisi ya siku 14 ili kulipa kodi hizo wanazodaiwa na endapo hawatalipa watafutiwa umiliki au mali zao kwa kupigwa mnada ili kufidia gharama wanazo daiwa.
Serikali kwa kutumia kampuni ya Udalali ya Msolopa Investment imeendesha oparesheni hiyo kwa kufika katika ofisi za wamiliki wa viwanja na mashamba makubwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Akiongea kwa kusisitiza, Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Yamungu Kayandabila amesema katika mwaka wa fedha 2016/17 Wizara imepanga kukusanya Sh. bilioni 111.77 kutokana na Kodi ya Pango la Ardhi.
Wizara haitaweza kufanikisha malengo hayo endapo itaendelea kuwaachia wadaiwa sugu ambao hawataki kulipa kodi. Kwani kwa miaka mingi sasa mapato mengi ya serikali yamekuwa yakiachwa kutokana na kushindwa kufuatilia wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi Kayandabila alisisitiza.
No comments