Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Akabidhi Msaada Wa Laptop

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi Laptop Mwandishi Chipukizi wa Vitabu vya Taaluma, Ali Salum Alujai ukiwa ni msaada aliompatia ili aweze kufanya vizuri zaidi katika uandishi wake. Makabidhiano hayo yalifanyika kwenye Ikulu ndogo ya Njombe.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

MAJALIWA:SERIKALI IMEANZA KULIPA MADENI YA WATUMISHI
*Jumla ya sh. bilioni 29 zililipwa mwaka jana

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imelipa jumla ya sh. bilioni 29 kwa watumishi mbalimbali wa umma wakiwemo walimu ikiwa ni sehemu ya madeni yao.

Alitoa kauli hiyo jana (Jumamosi, Januari 21, 2017) wakati akizindua vyumba vitatu vya kisasa vya madarasa katika shule ya sekondari Iwawa iliyoko wilayani Makete.

Waziri Mkuu alisema Serikali imedhamiria kumaliza madeni ya watumishi hao, ambapo hadi kufikia Novemba mwaka jana jumla sh. bilioni 29 zililipwa kwa watumishi 31,000.Alisema kwa sasa Serikali imejipanga kuhakikisha hakuna madeni mapya yanayozalishwa hivyo amewataka watumishi wa umma na wananchi kuendelea kuiunga mkono Serikali.

Hata hivyo alisema Serikali inaendelea na mikakati ya kuboresha sekta ya elimu kwa kujenga mazingira bora ya kufundishia na kujifunzia.“Tumeanza mradi wa ujenzi wa nyumba za walimu katika halmashauri nchini. Hapa Makete tumeleta sh. milioni 557 kwa ajili ya ujenzi huo,” alisema.

Alisema nyumba hizo za walimu zinazojengwa katika maeneo mbalimbali hususan ya vijijini ni za kisasa ambazo zinalenga kuwaondolea changamoto ya makazi.Waziri Mkuu alisema Serikali inafanya jitihada za dhati za kuhakikisha kila Mtanzania anapata elimu kwa kuwa elimu ni kichocheo cha maendeleo ya jamii.

“Tumedhamiria kumpatia elimu kila Mtanzania, hivyo halmashauri zihakikishe kila kijiji kinakuwa na shule ya msingi na lazima ziwe na darasa la awali,” alisema.Naye Mkuu wa Shule hiyo, Mwalimu Novatus Msivala aliishukuru Serikali kwa kugharamia ujenzi wa vyumba hivyo vitatu vya madarasa na matundu 10 ya vyoo pamoja na uingizaji wa maji kwenye vyoo na utengenezaji wa madawati 46.

Alisema ujenzi huo umegharimu sh. milioni 95 ambao utasaidia kupunguza msongamano kwa wanafunzi. Kwa sasa Serikali na wananchi wanaendelea kukamilisha ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na ofisi ya walimu.
                       
Katika hatua nyingine jana Waziri Mkuu alitimiza ahadi yake ya kumpatia laptop mwanafunzi Ally Alijai wa Chuo kikuu cha SAUT tawi la Songea mkoani Ruvuma.Ahadi hiyo aliitoa mwanzoni mwa mwezi huu alipokuwa katika ziara yake kikazi mkoani Ruvuma, lengo likiwa ni kuendeleza kipaji cha utunzi wa vitabu kwa mwanafunzi huyo.

Alisema mwanafunzi huyo alionyesha umahiri mkubwa katika utungaji wa kitabu ambacho kinaweza kutumika kufundishia katika shule za sekondari.

Hata hivyo Waziri Mkuu alisema tayari kitabu hicho kimeshawasilishwa Taasisi ya Elimu Tanzania (TEA) kuona kama kinaweza kuanza kutumika kwa kufundishia. Mwanafunzi huyo alishukuru kwa zawadi hiyo na kuahidi kutunga vitabu vizuri zaidi.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, JANUARI 22, 2017

No comments

Content by MwasebaINFO.All RIghts Reserved. Powered by Blogger.