Waziri mkuu atembelea bwawa la Mtera apiga marufuku uharibifu wa mazingira.

Waziri mkuu Kassim Majaliwa amewataka wakuu wa mikoa ya Singida, Mbeya, Iringa na Dodoma wawasimamie wananchi wao na kuhakikisha hakuna shughuli za kibinadamu zinazofanyika ndani ya vyanzo vya maji.

Ametoa kauli hiyo leo alipozungumza na watumishi wa kituo cha kuzalisha umeme cha Mtera alipotembelea bwawa la Mtera akiwa njiani kwenda mkoani Njombe kwa ziara yake ya kikazi.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo baada ya Kaimu Meneja wa Kituo cha kuzalishia umeme cha Mtera, Mhandisi Edmund Seif kutaja baadhi ya changamoto zinazokikabili kituo hicho kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa shughuli za kibinadamu ndani ya vyanzo vya maji.

Kufuatia hali hiyo Waziri Mkuu ameagiza vifanyike kwa vikao vya ujirani mwema ili wananchi waelimishwe umuhimu wa  kutunza vyanzo vya maji  na ni marufuku kuendesha shughuli za kibinadamu ndani ya kilomita 60 kutoka kwenye chanzo.

Awali, Mhandisi Seif alisema kituo hicho cha Mtera kinazalisha megawati 80 kwa siku ambazo zinaingizwa kwenye gridi ya Taifa. Alisema bwawa hili kwa sasa lina maji ya kutosha kuzalisha umeme hadi msimu ujao wa mvua.

Mhandisi hiyo alisema bwawa hilo linategemea kupata maji kutoka mto Ruaha Mkuu, mto Ruaha Mdogo na Vyanzo vyote hivyo vinaathiriwa na shughuli za kibidamu ambapo watu wanalima na kuingiza mifugo.

Baada ya kutoka kituoni hapo Waziri Mkuu alitembelea shamba la Igingilanyi ambalo ni moja kati ya mashamba matatu ya kufugia ng’ombe yanayomilikiwa na kiwanda cha kuzalisha bidhaa za maziwa ya Asas kilichoko mkoani Iringa.

Akiwa shambani hapo Waziri Mkuu aliwaagiza wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kuhakikisha wanasimamia vizuri mgawanyo wa ardhi ndani ya halmashauri zao pamoja na kusimamia mipaka kati ya wilaya na wilaya.

Pia aliwataka Maofisa Mifugo kuongeza kasi ya kutambua mifugo iliyoko kwenye maeneo yao na kuiwekea alama ili kuzuia uhamiaji holela wa mifugo kwa lengo la kuzuia migogoro kati ya wafugaji na wakulima.

Kwa upande wake mmoja wa Wakurugenzi wa kiwanda cha Asas, Bw. Fuad Abri alisema kiwanda hicho kina mashamba matatu yenye jumla ya ekari 2,000 na ng’ombe  1,010 kati ya hao 350 hukamuliwa maziwa na kutoa wastani wa lita 5,000 kwa siku.

Alisema katika mashamba hayo wameajiri wafanyakazi 175 na wamefanikiwa kutumia njia ya uhamilishaji (Artificial Insemination) katika mashamba yote na njia hiyo inawasaidia kuchagua jinsia ya ng’ombe wanayohitaji.

 

No comments

Content by MwasebaINFO.All RIghts Reserved. Powered by Blogger.