Walimu 7 waomba kuhama wakihofia maisha yao


KUTOKANA na kifo cha Mjumbe wa Serikali ya Kijiji cha Nyambunda, Kata ya Bungu wilayani Kibiti mkoani Pwani, Oswald Mrope kilichotokea hivi karibuni kwa kuuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiofahamika, walimu wanaofundisha kwenye shule za kijiji hicho, wameomba kuhamishwa kuhofia maisha yao.

Hofu hiyo imekuja baada ya walimu hao kuona kuwa kumekuwa na matukio kadhaa ya kuuawa kwa viongozi wa kijiji hicho, huyo akiwa ni kiongozi wanne kuuawa.

Akizungumza kwa njia ya simu na gazeti hili, Katibu wa Chama cha Walimu Wilaya ya Kibiti, Antony Mangwalu alisema walimu saba wanaofundisha shule mbili za kijiji hicho za Banduka, yenye walimu wanne na Mkandala, yenye walimu watatu wameiomba halmashauri kuwahamisha kutokana na matukio hayo.

Mangwalu alisema wauaji hao, wamekuwa wakifika kwenye kijiji hicho na kuwatafuta walengwa wao, kisha kufanya mauaji na kutoweka kusikojulikana.

Wamefanya hivyo kwa viongozi wa kijiji hicho na kwa sasa hakuna uongozi.

“Walimu hao wanatarajia kuandika barua kwa mwajiri wao ambaye ni mkurugenzi wa halmashauri ili wahamishiwe kwenye vituo vingine na shule hiyo ifungwe kuhofia kuwa wanaweza kufanyiwa vitendo hivyo kama wanavyofanyiwa viongozi wa kijiji hicho,” alisema Mangwalu.

Aidha, alisema mauaji hayo yalianza kwa Mwenyekiti wa Kijiji Aprili 24, mwaka jana, ikafuatiwa na Mtendaji wa Kijiji Oktoba 24, na Desemba tano mwaka jana, aliuawa Mwenyekiti wa Kitongoji na Januari 18 ndipo alipouawa Mjumbe wa Serikali ya Kijiji ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Shule.

“Alipouawa Mtendaji wa Kijiji ambaye alikuwa akiishi kwenye nyumba ya zahanati ya kijiji, wahudumu wa zahanati hiyo waliomba kuhamishwa na zahanati hiyo kufungwa wakihofia usalama wao ambapo na wao walitoa taarifa ya kuwa na hofu ya usalama wao,” alisema Mangwalu.

Katibu huyo wa CWT Kibiti alisema kutokana na kutokuwepo usalama wa kutosha kijijini hapo, ni vema na wao wakahamishiwa kwenye vituo vingine vya kazi kwenye wilaya hiyo.

Mjumbe huyo wa serikali ya kijiji hicho cha Nyambunda aliuawa Januari 18, kati ya saa mbili na saa tatu usiku baada ya watu sita kufika kijijini hapo na kumuua kwa kumpiga risasi tatu za usoni, kifuani na kwenye mbavu, kisha kutoweka na pikipiki yake.

Jitihada za kumpata Mkuu wa Wilaya ya Kibiti, Gulamhussein Kiffu hazikufanikiwa, kwani simu yake ilipopigwa iliita bila ya kupokelewa ili azungumzie suala hilo la walimu hao.


No comments

Content by MwasebaINFO.All RIghts Reserved. Powered by Blogger.