Uchache wa wahadhiri wazamivu waangusha umahiri wa wahitimu


LICHA ya kuwepo kwa jitihada nyingi zenye kuboresha elimu nchini, imeelezwa kuwa bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali na ikashauriwa kuwepo kwa haja ya wataalamu kuipitia kwa lengo la kuiboresha zaidi.

Aidha, imeelezwa kuwa asilimia 25 ya wahadhiri wa vyuo vikuu nchini ndio wenye elimu ya kiwango cha Shahada ya Uzamivu, jambo linalochangia vyuo kutozalisha wataalamu wenye uwezo stahiki.

Akizungumza jana Dar es Salaam katika uzinduzi wa Mpango Mkakati wa Shirika la HakiElimu wa Miaka Mitano (2017-2021), Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Kitila Mkumbo alisema kutokana na changamoto hizo, ipo haja ya kuwa na hatua za muda mfupi na muda mrefu ili kutatua matatizo ya elimu.

Profesa Mkumbo alisema kwa upande wa elimu ya juu, inakabiliwa na tatizo kubwa, lakini zaidi haina walimu waliobobea kwa ujumla wake wenye Shahada za Uzamivu ambapo ipo haja ya kufundisha walimu wengi zaidi.

“Hali ni mbaya zaidi katika elimu hususani kwa walimu wa vyuo vikuu ambapo katika vyuo vikuu vya Tanzania ni asilimia 25 pekee ndio yenye walimu wenye elimu ya Shahada ya Uzamivu, ukiondoa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambacho kina asilimia 41,” alisema Profesa Mkumbo.

Alisema hali ni mbaya katika hilo kwa kuwa UDSM inazidiwa na Chuo Kikuu cha Botswana ambacho kina wahadhiri wenye Shahada ya Uzamivu kwa asilimia 65 kikifuatiwa na chuo Kikuu cha Cape Town, Afrika Kusini kwa asilimia 63.

Vyuo vingine na idadi ya wahadhiri wenye Shahada ya Uzamivu kwenye mabano ni pamoja na Ghana kwa asilimia (50), Nairobi asilimia 46, Mauritius asilimia 42 na Makerere kwa asilimia 31.

Hata hivyo, alisema ipo haja ya kuwa na vyuo vya kikanda vilivyoboreshwa badala ya kuwa na mlolongo wa vyuo vingi nchini ikiwa ni kufikiria upya namna ya uendeshaji wa vyuo vikuu nchini, viwe na tija kwa miaka 20 ijayo.

Aidha, Profesa Mkumbo alimshukuru Rais John Magufuli kwa hatua ya kuwachukua walimu wenye kiwango hicho cha elimu na kuwapa kazi serikalini kutoka UDSM, lakini pia akaomba asaidie kuruhusu ajira kwa chuo hicho ili izibe pengo.

Kuhusu elimu ya msingi, alisema pamoja na jitihada nyingi zinazofanywa ina changamoto katika ubora wake ambao bado wanafunzi wanaozalishwa hawapati maarifa mazuri katika kujenga maisha.

Kuhusu Mpango Mkakati wa HakiElimu kwa miaka mitano ijao, Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, John Kalaghe alisema kupitia mkakati huo watashawishi mabadiliko ya sera na utekelezaji wake, kukuza ushiriki wa wananchi na kujishughulisha na kukuza uwazi na uwajibikaji.

No comments

Content by MwasebaINFO.All RIghts Reserved. Powered by Blogger.