Serikali yashtukia ubia na shule binafsi

Serikali yashtukia ubia na shule binafsi

WAMILIKI wa shule binafsi sasa wameomba kuingia ubia na Serikali ili wapewe ruzuku kuwezesha shule zao kudahili wanafunzi wa kidato cha kwanza, kwa maelezo kuwa shule hizo zitasaidia kuondokana na kero ya baadhi ya wanafunzi wanaofaulu kukosa nafasi katika shule za serikali.

Hata hivyo, Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi imekataa ombi hilo kwa maelezo kuwa serikali ina shule za kutosheleza mahitaji yaliyopo na haihitaji msaada wa shule binafsi katika kukabiliana na changamoto zilizopo katika suala la vyumba vya madarasa.

“Serikali hatuna mpango wa kuingia ubia na shule binafsi katika kudahili wanafunzi wa kidato cha kwanza, sisi tumeamua kutoa elimu bure na tumeboresha mazingira ya shule zetu, wao wanaendesha shule zao kwa kulipisha na waendeshe peke yao,” alisema Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Profesa Simon Msanjila.

Ombi la Tamongsco Kupitia Shirikisho la Wamiliki na Mameneja wa shule na Vyuo visivyo vya Serikali (Tamongsco), wamiliki hao wameiandikia Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi kuomba wizara iwashirikishe katika udahili wa wanafunzi 12,000 ambao wamefaulu mitihani ya darasa la saba mwaka jana, lakini kutokana na ukosefu wa madarasa hawataweza kwenda kidato cha kwanza.

“Kila mwaka tunaiomba Serikali ituondolee kodi, badala yake shule binafsi zipewe ruzuku ili watoto wanaokosa nafasi za kusoma katika shule za Serikali kila mwaka wapate elimu hiyo katika shule binafsi kwa mikataba maalumu ya ubia wa sekta ya umma na binafsi,” alisema Katibu Mkuu wa Tamongsco, Benjamin Nkonya katika barua yao waliyoiwasilisha wizarani.

Nkonya alisema baadhi ya madarasa katika shule zisizo za serikali hayana wanafunzi wakati madarasa katika shule za serikali yamefurika wanafunzi hadi 200 kwa darasa moja, jambo ambalo shule hizo binafsi zinaona kwamba ni kuwaweka katika mazingira mabovu kabisa ya kujifunzia na kufundishia wanafunzi hao.

Katibu Mtendaji huyo alisema kama Serikali inatoa ruzuku kwa hospitali binafsi, ifanye hivyo pia kwa shule binafsi za sekondari ili watoto wote wa kitanzania waweze kupata elimu kwa usawa. Majibu ya Serikali

Profesa Msanjila alisema kwamba Serikali imeamua kuboresha shule zake na kutoa elimu bure, jambo ambalo limewavutia wananchi wengi na sasa wanapeleka watoto wao katika shule za serikali tofauti na miaka ya nyuma.

Alisema kutokana na hali hiyo serikali haina mpango wa kuingia ubia na shule binafsi, badala yake itaendelea kutoa miongozo ya elimu inayoelekeza sera za elimu zinazotakiwa kufuatwa na shule ambazo sio za serikali na sio kuingia nazo ubia katika kudahili wanafunzi.

“Hawa tulitaka kuweka ada elekezi, lakini walitumia wanasiasa kupinga, kwa madai kwamba tunaingilia elimu ambayo serikali haihusiki, jambo hilo serikali imeamua kuachana na nalo ili soko liweze kuamua,” alisema Profesa Msanjila.

Aliongeza kuwa serikali imekuwa inaingia ubia katika sekta ya afya katika wilaya au mkoa ambako hakuna hospitali kubwa ya serikali na hivyo kulazimika kuingia ubia na hospitali binafsi au za mashirika ya dini zilizoko katika wilaya hizo.

“Sasa kwenye sekta ya elimu, serikali ina shule kila kata na kila kijiji, sasa huo ubia wanaotaka tuingie kwa sababu zipi? Hakuna sehemu ambako serikali haina shule,” alisisitiza Naibu Katibu Mkuu huyo.

Alisema baada ya kukataa ada elekezi, serikali iliona kuwa shule hizo zisizo za serikali zinafanya biashara na hazitoi huduma kama zinavyodai ndio maana zinalipa kodi zote zinatakiwa kulipwa na kampuni nyingine inayofanya biashara.

“Baada ya kukataa ada sisi tuliona kwamba hawa wanafanya biashara, hivyo lazima waendelee kulipa kodi maana hawatoi huduma,” alisema Profesa Msanjila.

Mtazamo wa Tamongsco Alisema Tamongsco inaona kwamba kuwasubirisha wanafunzi wengi hivyo kwa muda uliotajwa na serikali wa kujenga madarasa ndipo wajiunge na kidato cha kwanza kutasababisha malengo ya Matokeo Makubwa Sasa (BRN) kutofikiwa.

Katika andiko hilo ambalo limesainiwa na Katibu Mtendaji wa Tamongsco, wanadai kwamba ubia wa sekta ya umma na binafsi katika sekta ya elimu umeleta mafanikio makubwa nchini Uganda ambako serikali inatoa ruzuku kwa shule binafsi ambazo ni asilimia 80.

“Tuna ushahidi kwamba nchi nyingine nyingi duniani hutumia mifumo hii ya PPP na hufanikiwa kwa kiasi kikubwa kutoa elimu yenye ubora wa hali ya juu kwa gharama nafuu kuliko gharama ambayo serikali ingetoa bila kutumia mfumo wa PPP,” linasema andiko hilo la Tamongosco.

Wamiliki hao walisema kutokana na tofauti za wamiliki wa shule zetu, wamependekeza njia za ushirikiano kati ya sekta ya umma na isiyo ya umma zitumike katika kuondoa changamoto ya uhaba wa vyumba vya madarasa kwa ajili ya wanafunzi 12,422 waliokosa nafasi katika shule za serikali na wale watakaokosa kwa miaka ijayo.

Miongoni mwa njia hizo ni Mfumo wa Udahili Uliowianishwa ambao lengo lake ni kuondoa uwezekano wa mwanafunzi mmoja kudahili zaidi ya mara moja.

Kama ilivyo katika vyuo vikuu. Pia Serikali itenge kiasi cha fedha kwa mwanafunzi mmoja. Shule husika itatoza ada ya ziada kwa makubaliano na serikali.

Njia nyingine ni udhamini katika utaratibu huu, ikokotolewe gharama halisi ya kumsomesha mwanafunzi mmoja kwa mwaka katika shule ya serikali kwa kila kanda kwa kuzingatia nguvu ya fedha ya mahali husika na serikali itoe fedha hizo.

No comments

Content by MwasebaINFO.All RIghts Reserved. Powered by Blogger.