Mkakati Mpya wa Kumtoa Godbless Lema Gerezani
Chadema imeamua kuja na mpango mpya wa kuhakikisha Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema anatolewa mahabusu.
Lema amekuwa mahabusu tangu Novemba mwaka jana, lakini chama hicho kimesema sasa kinataka apate haki ya kisheria na kuwa huru kwa kuwatumia wanansheria katika kesi mbalimbali zinazomkabili.
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu amesema hayo baada ya yeye, mwenyekiti wake, Freeman Mbowe pamoja na viongozi wengine kumtembelea Lema mahabusu anakoshikiliwa tangu Novemba 2, mwaka jana kwa tuhuma za kutoa lugha za uchochezi dhidi ya Rais John Magufuli.
Lema amekuwa akikwama kupata dhamana kutokana na sarakasi za kisheria zilizosababisha upande wa utetezi uende hadi Mahakama Kuu katika kuhakikisha anapata haki hiyo, lakini hadi sasa bado vita hiyo ya kisheria haijaisha.
Lissu amewaambia waandishi wa habari mjini Arusha kwamba wataongeza nguvu ya mawakili wa Chadema katika kesi hiyo kila itakapokuwa ikitajwa mahakamani.
Pia, watakiandikia Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) barua rasmi kukitaka kitoe tamko kwa namna yoyote ili kiseme katika kesi ya Lema kipo upande upi na kama kikisema hakihusiki, basi hakutakuwa na chama cha wanasheria nchini na wakiona kuna hoja, basi watawataka watoe mawakili waliopo Arusha kusaidia kesi zinazomkabili Lema.
“Hawa wanasheria wasijidai hamnazo wakati mbunge wao yupo mahabusu. Tutawaambia wawepo mahakamani kwa kuwa wananchi wa kawaida hawaruhusiwi kuja kusikiliza kesi hiyo, basi wajae wanasheria,” amesema Lissu.
Awali, Mbowe amesema chama na viongozi waliamua kwenda kumuona Lema na familia yake kwa kuwa yupo mahabusu kinyume na haki za binadamu.
“Lema ana moyo mkuu sana na amejifunza mambo mengi kwa mujibu wa maelezo yake. Anasema wapo mahabusu asilimia 70 wenye makosa yanayostahili kupewa dhamana, lakini hawajapewa,” amesema.
No comments