Kipigo cha Wanajeshi cha Sababisha Kifo cha Konda wa Daladala..!!
Kondakta wa daladala linalofanya safari zake kati ya Nguvumali hadi Raskozone, Salim Kassim amefariki dunia baada ya kudaiwa kushambuliwa ndani ya kambi ya jeshi jijini hapa.
Kwa mujibu wa habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba, kondakta huyo alikufa wakati akipelekwa katika Hospitali ya Mkoa ya Bombo na chanzo cha kifo bado kinachunguzwa.
Mwananchi ilielezwa kuwa tukio hilo lilitokea juzi usiku, ambapo mashuhuda walidai kuona kondakta huyo akichukuliwa na wanajeshi na kuingizwa kambini na baadaye alitolewa akiwa hajitambui
Akizungumzia tukio hilo, Khalid Juma mkazi wa Nguvumali jijini hapa alisema askari hao wamekuwa na desturi ya kuwapiga wananchi bila kuchukuliwa hatua zozote za kisheria.
“Tumekuwa tukipata vipigo kila wakati, licha ya viongozi kupata taarifa za matukio hayo wamekaa kimya na hili tukio ni la tatu kutokea hapa,” alidai Khalid.
Diwani wa Kata ya Nguvumali ambaye pia ni Meya wa Jiji la Tanga, Alhaji Mustapha Selebosi alisema sababu za kipigo hicho ni mwanafunzi wa shule moja jijini Tanga ambaye ni mtoto wa ofisa wa JWTZ kuzozana na kondakta.
No comments