Jeshi la polisi lakamata 11
Jeshi la polisi lakamata Mangariba 11
Jeshi la polisi kanda maalum ya Tarime na Rorya mkoani Mara, limefanikiwa kuwakamata mangariba kumi na moja wilayani Tarime kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya uwakeketaji watoto wa kike zaidi ya 800 katika wilaya ya Tarime kinyume cha sheria.
Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Tarime Bw. Glorious Luoga,akizungumza wakati wa watoto wa kike zaidi ya 300 wakihitimu mafunzo juu ya madhara ya ukeketaji baada kuzikimbia familia zao kwa kuogopa kukeketwa, amesema watoto hao wamekeketwa katika kipindi cha mwezi disemba mwaka jana na kwamba vyombo vya dola vinaendelea na msoko wa mangariba wengine wanao daiwa pia kuhusika kufanya ukatili huo.
Naye katibu mkuu wa wizara afya, maendeleo ya jamii,jinsia,wazee na watoto Bi. Sihaba Nkinga, akizungumza wakati wa hafla hiyo katika kituo cha Masanga wilayani Tarime, amesema kuwa kila mwaka duniani watoto wa kike zaidi ya milioni mbili wako katika hatari ya kukeketwa, Tanzania ikiwa ni miongoni mwao.
Kwa upande wake mwakilishi wa askofu wa kanisa katoliki jimbo la Musoma linalomiliki kituo hicho Padri Ernest Kamugisha, ameupongeza uongozi wa serikali wilayani Tarime kwa jinsi unavyopambana na vitendo hivyo vya ukeketaji kwa watoto wa kike,licha ya vikwazo vingi vinavyotolewa na wazee wa mila wakiwemo baadhi ya viongozi wa kiasiasa katika wilaya ya tarime.
No comments