JANUARY 6, 2017 Dk Nchimbi amfutia shtaka la Sh1 bilioni kada wa CCM
Balozi Mteule, Dk Emmanuel Nchimbi (Kushoto) na kada wa CCM James Mwakibinga (Kulia).
Dar es Salaam. Balozi Mteule, Dk Emmanuel Nchimbi amepokea ombi la kuombwa msamaha kutoka kwa kada wa CCM James Mwakibinga aliyemtuhumu kujimilikisha sehemu ya jengo la Umoja wa Vijana wa CCM, mwishoni mwa mwaka jana.
Dk Nchimbi kupitia kwa wakili wake, Silvanus Mayenga kutoka FK Law Chambers alimfungulia Mwakibinga shauri la madai Na.300 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, akitaka amlipe fidia ya Sh1 bilioni kwa kumchafulia hadhi yake mbele ya jamii ikiwa pamoja na kumtuhumu kuuza viwanja 200 vya UVCCM vilivyoko Temeke.
Akizungumza na waandishi wa habari leo (Ijumaa) jijini Dar es Salaam, Mwakibinga amesema madai hayo aliyatoa baada ya kupata taarifa kutoka kwenye vyanzo visivyo rasmi lakini aliziamini akiona ni jambo la kizalendo kupaza sauti ili hatua zichukuliwe.
“Naomba kukiri kuwa taarifa hizi nilizipata kutoka vyanzo visivyo rasmi na kwa bahati mbaya nikaziamini na nikaona ni jambo la kizalendo kupaza sauti ili hatua zichukuliwe.”
Amesema baada ya kufanya utafiti wa kutosha amejiridhisha vya kutosha kuwa Dk Nchimbi hamiliki na hajawahi kumiliki sehemu yoyote ya jengo la UVCCM na kuwa umoja huo haujawa kumiliki viwanja eneo lolote wilayani Temeke.
Baada ya kupokea ombi hilo wakili wa Nchimbi amesema, “Nitawasiliana na mteja wangu tuangalie jinsi ya kuliondoa shauri hilo mahakamani.”
No comments