Jambazi auawa akijaribu kuwatoroka polisi
MTU mmoja mwanaume ambaye amejulikana kwa jina moja la Mungiki (35) ameuawa kwa kupigwa na risasi na askari polisi wakati akijaribu kuwatoroka baada ya kukutwa akiwa na silaha aina ya bastola yenye namba za usajili TZCAR 97076.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza Ahmed Msangi alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea Januari 27, mwaka huu saa 6.30 usiku katika Mtaa wa Bwiru Kata ya Kitangiri katika Manispaa ya Ilemela.
Alisema bastola aliyokamatwa nayo aliipora kwenye tukio la unyang’anyi wa kutumia silaha mwaka 2013 mkoani Tabora. Alisema polisi walipata taarifa kutoka kwa raia wema juu ya kuwepo kwa kijana anayejihusisha matukio ya uhalifu wa kutumia silaha jijini Mwanza na mikoa jirani.
“ Polisi walifanya ufuatiliaji wa tukio hilo, na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa na baada ya kuhojiwa alikiri kuwa na silaha hiyo na ndipo alipowaongoza askari hadi maeneo ya Songambele mtaa wa Kabohoro kwenye mapango ya mawe na kuikuta bastola hiyo ikiwa imefichwa kwenye pango la jiwe,” alifafanua.
Alisema mtuhumiwa alikiri kupewa bunduki na mtu mmoja ( jina limehifadhiwa kwa sababu za kiusalama) ambaye walikuwa wakishirikiana kwenye matukio mbalimbali ya unyang’anyi wa kutumia silaha jijini Mwanza na mikoa jirani.
Alisema mtuhumiwa alisema walishirikiana na mwenzake huyo katika kuvamia kwenye maduka mawili yanayofanya miamala ya fedha katika maeneo ya Kilimahewa kwa Msuka na kupora vitu mbalimbali kwa kutumia silaha hiyo na kufunguliwa kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha yenye namba MZN/IR/632/2017.
“Askari waliongozana hadi kwenye alikokuwa ameficha silaha, lakini ghafla mtuhumiwa alikurupuka akiwa na pingu mkononi na kuanza kukimbilia upande wa pili wa barabara kwa lengo la kutoroka. “Askari walifyatua risasi kadhaa hewani wakimuamuru asimame lakini alikaidi na ndipo walifyatua risasi wakimlenga kwenye miguu lakini kwa bahati ilimpiga sehemu za juu za kiuno, ambapo mtuhumiwa alikufa akiwa njiani kuelekea hospitalini,” alifafanua.
No comments