BILLICANAS YA MBOWE YAANZA KUBOMOLEWA RASMI
BILLICANAS YA MBOWE YAANZA KUBOMOLEWA RASMI
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limeanza kubomoa jengo la iliyokuwa Klabu Bilicanas na ofisi za Free Media inayomiliki gazeti la Tanzania Daima zinazomilikiwa na Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Taifa, Freeman Mbowe, lililopo makutano ya barabara ya Mkwepu na Indira Gandhi lenye kitalu namba 725-726/24 na hati namba C. T No. 186018/15 and C. T No. 186018/10.
Ubomoaji huo ulioanza jana unafanyika wakati Mbowe ameingia katika mgogoro na NHC baada ya kampuni ya udalali ya Poster and General Traders kumtolea vyombo nje mwanzoni mwa Septemba, mwaka jana kwa kudaiwa Sh bilioni 1.2 ambayo ni deni la pango ya miaka 20.
Mwanzoni mwa Septemba, mwaka jana NHC kwa kushirikiana na Kampuni ya Poster and General Traders, ilifika katika jengo hilo kwa maelekezo ya kutoa thamani mbalimbali zilizokuwa katika ofisi za jengo hilo na kumpa Mbowe siku 14 kulipa deni analodaiwa na kuweza kugomboa mali hizo.
Mpango huo ulisimamiwa na Meneja wa Ukusanyaji Madeni wa NHC, Japhet Mwanasenga na alisema Mbowe alikuwa na muda wa wiki mbili kwa wakati huo kulipa fedha hizo kabla ya vifaa vyake kupigwa mnada.
Mwanasenga alisema taratibu zote zilifuatwa kabla ya kumwondoa mteja huyo ikiwamo notisi na kwamba vifaa hivyo vitashikiliwa kwa muda huo na endapo akishindwa kulipa jengo hilo atapangishwa mtu mwingine.
Alisema shirika hilo linahitaji fedha kwa ajili ya ujenzi na uendelezaji wa majengo yake hivyo mteja anayedaiwa ajiandae kuondolewa wakati wowote huku baadhi ya watu wakilihusisha tukio la Mbowe kuondolewa katika ofisi hizo na masuala ya siasa.
Hata hivyo, Mwanasenga, alisema uamuzi wa kumwondoa katika ofisi hizo hauna uhusiano na masuala ya siasa.
Kutokana na hali hiyo, Mbowe kupitia Mawakili wake, John Malya na Peter Kibatala, walifungua shauri la kupinga kuondolewa katika jengo hilo Mahakama Kuu ya Tanzania na kutaka kurudishwa katika jengo hilo.
Hata hivyo, maombi hayo yalitupiliwa mbali Oktoba 17, mwaka jana na Jaji Sivangilwa Mwangesi na kusema kuwa mahakama hiyo imechukua uamuzi huo baada ya kujiridhisha na hoja kuu tatu kuwa hakuna mkataba wa ubia uliopo baina ya NHC na Mbowe Hotels Limited na kuwa uhusiano pekee uliosalia ni wa mpangaji na mpangishaji.
Pia Jaji Mwangesi alisema mahakama imejiridhisha kuwa NHC imefuata taratibu zote katika kuiondoa Mbowe Hotels Limited kwa kutoa ilani ya siku 30 na baadaye siku 14 kabla ya kumtoa mteja wao huyo.
Kuhusu kusajiliwa au kutosajiliwa kama dalali rasmi wa mahakama wa kuendesha mchakato wa kumhamisha Mbowe katika jengo hilo, alisema hiyo nayo haikuwa hoja yenye mashiko na kwamba waombaji walitakiwa kuwasiliana na Msajili wa Mabaraza ya Ardhi.
Katika shauri hilo, NHC iliongozwa na Wakili Kiongozi, Aloyce Sekule na Ipilinga Panya na mawakili wake wengine waliojikita katika kujibu hoja zilizokuwa zikitolewa na wateja wao.
No comments